Kauli yake imeweka bayana mkakati mpya wa kifedha na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa, akitangaza rasmi kwamba Tanzania sasa itajitegemea zaidi na kutotegemea mikopo ya nje kwa asilimia kubwa.
Rais Samia alifunguka kuhusu ugumu wa kifedha unaoikabili nchi, akihusisha hali hiyo na matukio ya ndani ya nchi ambayo yameathiri sifa ya Tanzania katika macho ya taasisi za kifedha za kimataifa.
"Changamoto inayotukabili ni rasilimali zetu ni chache. Mambo mengi tunategemea kupata kutoka nje, mikopo kutoka Taasisi mbalimbali za Kimataifa, mabenki ya Kimataifa. Lakini yaliyotokea nchini kwetu yametutia doa kidogo, kwahiyo huenda yakatupunguzia sifa ya kupata mikopo kwa urahisi kama tulivyopata muhula wa kwanza... Doa tulilojitia huenda likaturudisha nyuma.”
Kauli hii inatafsiriwa kama ishara ya mabadiliko ya vipaumbele vya kimkakati, kufuatia kushuka kwa uwezo wa kupata mikopo.

