Jumanne , 16th Dec , 2014

Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Khalist Luanda amesema kuwa changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa linaonyesha kuwa wananchi wamepata mwamko mkubwa wa kushiriki katika chaguzi.

Wananchi wakiwa kwenye foleni ya kuelekea kupiga kura katika chaguzi wa Serikali za Mitaa.

DODOMA.
Luanda alitoa kauli hiyo leo wakati akizungumza East Africa Radio kuhusiana na kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa ofisini kwake mjini Dodoma.

Alisema changamoto hizo zimejitokeza kutokana na idadi kubwa ya wananchi kujiandikisha katika uchaguzi huo na ndiyo maana sehemu nyingine walilazimika kuahirisha kufanya uchaguzi kutokana na kasoro mbalimbali.

Alisema changamoto ya watu kupiga kura mara mbilimbili kutokana na kukosekana kwa wino wa kuwatambulisha kama wamepiga kura ilitokana na uchaguzi huo kufanyika ngazi ya vitongoji, mitaa na vijiji ambapo watu wengi wanaoishi katika eneo moja kufahamiana kwa sura na ukoo wao kwa kuwa wanaishi pamoja.
Hivyo hawakuona umuhimu wa kuweka wino huo.

Hata hivyo amesema kuwa matokeo rasmi ya uchaguzi huo kwa nchi nzima atayatoa leo saa kumi jioni kutokana na vituo vingi kutowasilisha matokeo hayo mapema.

GEITA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Geita, kimepata pigo baada ya mshindi wa nafasi ya ujumbe wa viti maalum katika uchaguzi uliofanyika jana Jumapili katika mtaa wa Msalala Geita mjini, Bertha Chimani miaka 32, kukutwa katika shimo la choo lisilotumika akiwa amefariki dunia.

Chimani ambaye alipata kura nyingi katika uchaguzi huo, aliwaaga wenzake waliokuwa wakisubiri kushangilia ushindi huo akiwamo dada yake kuwa anakwenda kujisaidia lakini hakuweza kurejea mpaka mwili wake ulipogundulika jana asubuhi.

Mwili wake ulikutwa ukielea katika shimo la choo kilichokuwa hakijafunikwa ndani ya uzio wa jengo lililokuwa linatumika kwa ajili ya kupigia na kuhesabia kura lenye kina cha zaidi ya futi 30.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai marehemu alitumbukia katika shimo hilo usiku na mwili wake uliopolewa na kikosi cha Zima Moto na kuhifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya wilaya ya Geita kwa uchunguzi zaidi.

Katika tukio lingine lililotokea leo, Simeo Isaka miaka 42, mkazi wa kijiji cha Ngokolo kata ya Bukomela tarafa ya Mweli wilayani Kahama, ameuawa kwa kukatwa na jembe kichwani wakati akishangilia matokeo ya ushindi wa chama chake cha CHADEMA.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Justus Kamugisha, amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo wakati Isaka akishangilia matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa kijiji cha Ngokolo.

ARUSHA.
Jiji la Arusha limetangazwa kufanyika upya kwa uchaguzi katika mitaa mitatu, hii ni kufuatia dosari zilizo jitokeza ikiwa ni pamoja na hali ya vurugu katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika kote nchini hapo jana .

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mkurugenzi wa jiji la Arusha Juma Idd ambaye pia ndiye msimamizi mkuu wa uchaguzi amesema katika baadhi ya mitaa ikiwemo Oyster Bay katika kata ya Unga Limited kulitokea hali ya vurugu jambo ambalo lilisababisha kuvurugika kwa kura hivyo kutangaza kufanyika kwa uchaguzi hapo kesho.

Ameongeza kuwa katika mtaa wa Old Police Line uchaguzi utafanyika wa wajumbe wawili mchanganyiko na mtaa wa AICC kwa wajumbe viti maalamu kufuatia kura za wajumbe kuwa sawa hivyo kukosa mshindi wa nafasi hizo.

Mkurugenzia amekiri kuwa changamoto kubwa waliyokabiliana nayo ni mchanganyiko wa majina jambo ambalo amesema linatokana na majina kufuata alfabeti jambo ambalo limekuwa gumu kwa wananchi wa kawaida kuweza kupata majina yao kiurahisi.

Nao baadhi ya wakazi wa jiji la Arusha wamekuwa na maoni tofauti kuhusu uchaguzi huo uliohusisha mitaa 154 ya jiji la Arusha.

Katika uchaguzi huo katika ngazi ya wenyeviti wa mitaa chama cha mapinduzi CCM kimepata mitaa 78, Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kipata mitaa 75 huku chama cha ACT, NCCR MAGEUZI kutoka pasipo kupata chochote.

NJOMBE.
UCHAGUZI wa serikali za mitaa uliofanyika juzi umegundulika kuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kutoonekana kwa majina na kusababisha wapigakura kuchukua muda mrefu wakati wa kupiga kura na kusababisha watu kuweza kupiga kura mara mbili kwa kutokuwa na vitambulisho.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Njombe Katibu wa CCM Mkoa wa Njombe, Hosea Mpagike, alisema kuwa uchaguzi huu umeonekana kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mpigakura kutoshika namba yake na kushindwa kuona jina lake katika karatasi za nje na kuingia ndani kufanikiwa kuliona.

Mpagike alisema kuwa uchaguzi huo umeenda vizuri bila ya kukutwa na changamoto nyingine yoyote mbali na hiyo ya kutoona majina nje.

Alisema kuwa tume ya uchaguzi huo ihakikishe kuwa uchaguzi mwingine kama huo unatakiwa kuwa na uandikishaji ambao utaweza kuwasaidia wapigakura kuto weza kujirudia mara mbili.

“Waandishi katika uchaguzi huu tumekuta malalamiko mengi ambapo waliokuwa hawayaoni majina yao nje na katika karatasi ya msimamizi ndani walikuwa wanayakuta” alisema Mpagike.

Akizungumzia matokeo ya uchaguzi kwa mkoa wa Njombe alisema kuwa katika wilaya ya Njombealisema kuwa kuna vijiji 108 na vijiji saba havikufanya uchaguzi na kati ya vijiji vilivyo fanya uchaguzi CCM imepata vijiji 94 sawa na Asilimia 93 na CHADEMA kimechukua vijiji 8 sawa na asilinia 7.44.

Alisema kuwa katika halmashauri ya Njombe na Makambako kuna jumla ya mitaa 82 ambapo CCM imechukua mitaa 54 sawa na asilimia 66 ambapo CHADEMA imechukua mitaa 28 ambapo ni sawa na aslimia 34 na chama cha NCCR Mageuzi imechukua kijiji kimoja.

Aliongeza kuwa katika halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe kulikuwa na vijiji 108 ambapo vijiji 4 havikufanya uchaguzi na katika CCM imechukua vijiji 102 sawa na asilimia 98.1 na CHADEMA imechukua vijiji 2 sawa na asilimia 1.9.

Katika halmashauri ya wilaya ya Ludewa Chama cha CCM kimefanikiwa kuchukua jumla ya vijiji 77 ambapo vijiji 4 havikufanya uchaguzi na kuwa CCM imechukua vijiji 64 sawa na asilinia 97 na CHADEMA imechukua vijiji 9 sawa na asilimia 3.

Aidha Mpagike alisema kuwa kiujumla uchaguzi umeenda vizuri na kuwa katika halmashauri ya wilaya ya Makete matokeo bado hayajamfikia na atatoa taarifa kama yatatoka matokeo hayo.

TABORA.
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina Batholomeo Edward mkazi wa mtaa wa majengo mjini Nzega mkoani Tabora amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi na askari wa jeshi la polisi wakati wakisubiri matokeo ya uchaguzi baada ya kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika jana kote nchini.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali ya serikali ya wilaya ya Nzega Dkt. Joseph Bahati amesema hospitali yake imepokea majeruhi wawili majira ya saa 11.00 Alfajiri mmoja akiwa amejeruhiwa tumboni na kitu chenye ncha kali kilichotoa utumbo wake na mwingine ubavu na mkono wa kushoto na kuwa wakiwa wanapewa matibabu mmoja wao akafariki dunia kutokana na kutokwa damu nyingi.

Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo limetokea majira ya saa 10.00 Alfajiri katika mtaa wa Majengo ambapo baadhi ya wakazi wa eneo hilo wakiwa wakisubiri matokeo msimamizi wa uchaguzi alimtangaza mgombea wa CCM, kuwa mshindi hali iliyosababisha taharuki miongoni mwa vijana na hivyo askari wa jeshi la polisi kuingilia kati na kuanza kuwatawanya kwa kupiga mabomu ya machozi hewani na baadaye kupiga risasi za moto na kuwajeruhi Batholomeo Edward na Lucas Daudi ambao wanadaiwa kuwa ni wafuasi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (ukawa).

Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) Wilayani Nzega wamelaani vikali kitendo cha jeshi la polisi kutumia silaha za moto kuwatawanya watu waliokuwa wakishangilia ushindi na hatimaye kusababisha mauaji hayo na kuwa suala hilo watalifikisha kwenye vyombo vya sheria ili iweze kuchukua mkondo wake.

Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora Bi. Suzan Kaganda amethibitisha askari wa jeshi lake kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto zilizopigwa juu kutawanya mkusanyiko wa watu waliokuwepo eneo hilo.