Waziri wa Kazi na Ajira Bi. Gaudensia Kabaka.
Msemaji wa Wizara hiyo Bw. Ridhiwani Wema, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akitangaza uamuzi wa serikali wa kutoa leseni za usajili wa makampuni ya uwakala wa ajira.
Kutangazwa kwa usajili mpya wa kampuni za uwakala na huduma za ajira kunafuatia kuisha kwa zuio lililowekwa na serikali dhidi ya kampuni hizo ambazo baadhi yake zilikuwa zinatuhumiwa kukiuka taratibu za uwakala wa ajira.
Wema amesema makampuni ambayo yamepatiwa usajili wa kufanya kazi ya uwakala wa ajira, hayatakiwi kufanya kazi zilizo nje ya majukumu waliyopewa ikiwemo kupokea mishahara na stahiki nyingine za ajira kwa niaba ya watu waliowatafutia kazi kwani stahiki za ajira ni mkataba wa pande mbili na sio tatu kama baadhi ya makampuni yalivyokuwa yanafanya.
Akifafanua kipengele hicho, Wema amesema baadhi ya makampuni yamekuwa yakijitangaza kutafutia watu ajira lakini badala yake zimejigeuza kuwa waajiri kwa niaba ya kampuni hizo ambapo mishahara ya waliowatafutia kazi hupitia kwao na kuanza kuipunguza, kitendo alichodai kuwa ni kinyume na taratibu za ajira.