Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu ambapo pia amewahakikishia wakazi wa wilaya ya Busega kuwa serikali itamaliza migogoro yote ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji wilayani humo.
Kauli hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Busega Rafaeli Chageni kuwasilisha kilio cha wananchi kukosa sehemu ya kulima kutokana na wawekezaji kuchukua maeneo makubwa kinyume na taratibu na wengine kughushi nyaraka za umiliki wa ardhi.
Waziri Majaliwa amewataka Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Jumanne Maghembe, Waziri wa TAMISEMI, Mhe. George Simbachawene, Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi, na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mwigulu Nchemba kutatua mgogoro huo.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watumishi na watendaji wote wa serikali wahamie yalipo makao makuu ya wilaya ya Busega kuanzia sasa ili kuleta kasi ya utendaji kazi kwenye wilaya hiyo ambayo ni mpya wafanye mapitio ya maeneo yote yenye migogoro ya ardhi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi waliofika kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi kwenye jengo la utawala la halmashauri ya wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Waziri Mkuu ambaye ameanza ziara ya siku sita ya mkoa huo atakagua shughuli za maendeleo na kusalimia na wananchi katika wilaya zote za mkoa huo.
Waziri Mkuu alisema kitendo cha watumishi kuhamia yalipo makao makuu ya wilaya kitasaidia kuongeza kasi ya kuleta maendeleo kwani watakuwa wanaziona changamoto zilizopo mahali wanapoishi.