Jumatano , 3rd Dec , 2014

Mkuu wa wilaya Uyui mkoani Tabora Bibi. Lucy Mayenga, ameishauri wizara ya afya na ustawi wa jamii kutambua fursa zinazotolewa na wahisani na kuchukua hatua za makusudi ili kutoa kibali kwa ajili ya kuanzishwa kituo cha afya cha Ilolangulu

Lucy Mayenga, Mkuu wa Wilaya ya Uyui

Mkuu wa wilaya Uyui mkoani Tabora Bibi. Lucy Mayenga, ameishauri wizara ya afya na ustawi wa jamii kutambua fursa zinazotolewa na wahisani na kuchukua hatua za makusudi ili kutoa kibali kwa ajili ya kuanzishwa kituo cha afya cha Ilolangulu, ili kuwanusuru wananchi ambao wamekuwa wakihangaika kufuata huduma zaidi ya kilometa 30.

Akizungumza na EATV katika zahanati ya ilolangulu inayolengwa kubadilishwa kuwa kituo cha afya, ambayo imepewa vifaa tiba vya kisasa kutoka mradi wa milenia, vikiwemo vya upasuaji mkubwa na mdogo, ambavyo vimekaa bila kutumika, kwa muda mrefu, Bi Lucy Mayenga amesema kuwa, ifikie wakati serikali iwatambue changamoto za afya zinazowakabili wananchi.

Awali akizungumzia hatua iliyofikiwa ya kuongeza vifaa meneja wa kijiji cha Milenia chenye vijiji 15 Dokt Guson Nyadzi amesema kuwa, kutokana na vifaa kuongezeka vimekuwa vikihamishiwa katika hospitali ya rufaa ya kitete, hata hivyo mradi wa milenia umeendelea kujenga majengo muhimu ili kukidhi matakwa ya kituo cha afya.

Wilaya ya Uyui mkoani Tabora yenye jiografia ya kuzunguka wilaya ya Tabora mjini, ina kutuo cha afya kimoja, ambapo wananchi hupata changamoto ya kufuata huduma za afya katika hospitali ya mkoa na wengine wilayani Nzega na Urambo.