Jumanne , 24th Mar , 2015

Watanzania wametakiwa kutowanyanyapaa watu wanaougua ugonjwa wa kifua kikuu kwani kitendo hicho hakiwezi kumaliza maambukizi ya ugonjwa huo na badala yake wawashauri na kuwaonesha mahali wanapoweza kupata tiba sahihi ya ugonjwa huo.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayojishughulisha na kampeni ya kupambana na ugonjwa wa UKIMWI na kifua kikuu ya MUKUKUTE, Bw. Joseph Mapunda, wakati wa zoezi la utoaji bure ushauri na huduma za kifua kikuu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kifua kikuu.

Mapunda amesema unyanyapaa umekuwa ukichangia kasi ndogo katika kukabiliana na ugonjwa huo, huku akiwataja watumiaji wa dawa za kulevya kuwa ndio walio katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya kifua kikuu huku mrundikano katika vyombo vya usafiri nao ukitajwa kuchangia maabukizi ya ugonjwa huo.

Kwa upande wao, waathirika wa kifua kikuu kutokana na matumizi ya dawa wa kulevya wameitaka serikali kuwapatia huduma na mahitaji ya msingi ili waweze kupona kifua kikuu na kuacha kutumia dawa za kulevya ili iwe mfano kwa wenzao ambao bado wanatumia dawa za kulevya waache na kuepuka kupata maambukizi ya kifua kikuu.

Awali Katibu mkuu wa wizara ya Afya na Ustawi wa jamii Dkt Donan Mmbando aliesema kuwa utafiti unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 30 ya vifo vya watu walioathirika na Ukimwi vinatokana na Ugomjwa wa Kifua Kukuu na inakadiriwa kuwa tangu kuanza kwa ugonjwa wa ukimwi, kati ya asilimia tano (5) hadi 10 ya watu wenye VVU wana ugonjwa wa kifua kikuu na takribani ya asilimia 40 wanaouguwa kifua kikuu wana maambukizo ya VVU.

Dk. Mmbando amesema, Tanzania ni nchi ya Sita katika bara la Afrika kwa kuwa na wagonjwa wengi wa kifua kikuu na takwimu za Wizara ya Afya ziligundua kuwepo kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu zaidi ya 65,000 kwa mwaka 2013,utafiti wa mwaka 2012 wa kutathimini kiwango cha ugonjwa huo,ulionyesha kuwa idadi kubwa ya watu wenye umri wa zaidi ya miaka 50 wapo katika hatari ya kupata ugonjwa huo.

Aidha amesema Kifua Kikuu ni ugonwa unaoambukiza na unasababishwa na vimelea aina ya bacteria na mtu anayeugua ugonjwa huo ni rahisi kuambikiza kwa watu wengine kwa kukohoa au kupiga chafya.

Dk. Mmbando aliendelea zaidi kwa kumesema kwa sasa takribani zaidi ya watu milioni 1.5 duniani wanafariki kwa ugonjwa wa kifua kikuu kila mwaka na asilimia kubwa ya vifo hivyo vinatokea katika nchi za Kusini mwa Jangwa la sahara na Tanzania ni kati ya nchi 22 yeye idadi kubwa ya wagonjwa wa kifua Kikuu Duniani. nchi hizo zinachangia asilimia 80 ya wagonjwa wa kifua kikuu ulimwenguni