Jumatano , 7th Apr , 2021

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewashukuru Watanzania wote kwa kuonesha mshikamano na uzalendo wa hali ya juu wakati wa kutangazwa na kipindi chote cha maombolezo ya msiba hadi mazishi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 7, 2021) alipozungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa ndege wa Dodoma akitokea Visiwani Zanzibar katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Abeid Aman Karume.

Machi 17, 2021 aliyekuwa Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan majira ya saa 5.15 usiku aliwatangania wananchi kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. Magufuli kilichotokea saa 12.00 jioni katika hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam.

Baada ya kutangaza taarifa za kifo hicho pia alitangaza siku 21 za maombolezo pamoja na taratibu za kuuaga mwili na mazishi, ambapo Machi 20 na 21, 2021 viongozi na wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani walipata fursa ya kuaga katika uwanja wa Uhuru.

Machi 22 yalifanyika mazishi ya Kitaifa Makao Makuu ya nchi jijini Dodoma ambayo yaliongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na viongozi kutoka nchi mbalimbali wakiwemo Marais tisa, Machi 23 zoezi la kuaga lilifanyika kwa wananchi wa Zanzibar.

Machi 24 wananchi wa mkoa wa Mwanza walipata fursa ya kuaga mwili wa Hayati Dkt. Magufuli, Machi 25 wananchi wa mkoa wa Geita walimuaga katika Uwanja wa Magufuli wilayani Chato na Machi 26, 2021 alizikwa nyumbani kwake Chato, Geita

Waziri Mkuu amesema anawashukuru Watanzania wote kwa namna walivyoshiriki katika zoezi hilo, hivyo amewaomba waendeleze utulivu na mshikamano mkubwa waliounesha katika kipindi chote cha majonzi. ”Wakati wote tangu msiba ulipotangazwa Watanzania walikuwa watulivu hadi leo tunapomaliza siku 21 za maombolezo, tunawashukuru sana.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa miongozo yake aliyoitoa ambayo iliiwezesha kamati ya mazishi ya kitaifa kuratibu vizuri zoezi hilo na kufanikisha mazishi ya Hayati Dkt. Magufuli. ”Kauli yake iliwasaidia Watanzania kuendelea kuwa watulivu huku wakimuombea Hayati Dkt. Magufuli.”