Jumatano , 9th Dec , 2015

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema zoezi la usafi lililofanyika leo nchini kote lisiishie hapo bali liwe endelevu ili Tanzania iwe na taswira nzuri kwa wageni wanaoingia nchini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Ametoa wito huo leo (Jumatano, Desemba 9, 2015) kwenye soko la Kariakoo wakati akishiriki zoezi la kufanya usafi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli la kutaka maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru yasiwepo, na badala yake watu wote washiriki kufanya usafi katika maeneo mbalimbali.

Waziri Mkuu Majaliwa pia amewataka viongozi wa soko la Kariakoo wafike ofisini kwake Jumatatu ijayo (Desemba 14, 2015) saa 4 asubuhi ili wamueleze wana mikakati gani ya kuboresha utoaji huduma kwenye soko hilo.

"Natambua kuwa siyo sahihi kupanga chini biashara tulizonazo, nataka hawa viongozi waje wanieleze wana mpango gani endelevu wa kuboresha soko hili," alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.

Waziri Mkuu ambaye alienda kufanya usafi kwenye soko hilo, alilazimika kuzungumza na mamia ya wananchi waliofika kushiriki zoezi hilo huku akikagua maeneo mbalimbali ya soko hilo hadi shimoni, na kusema aneridhika na usafi uliofanyika.

"Kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais Magufuli ya HAPA KAZI TU inatupa ari ya kufanya kazi, fanyeni kazi, watanzania mko huru kufanya kazi yoyote lakini cha msingi fuateni taratibu na kanuni, serikali hii tumeamua kuwajali watu wa chini, tutahakikisha wajasiriamali wadogo, akinamama lishe na wamachinga mnafanya kazi kwa amani na utulivu, " alisema.

Rais Magufuli aliamua kuitangaza siku ya leo (Desemba 9, 2015) ambayo ni maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru iwe ni siku ya kufanya usafi nchi nzima ili kuepukana na magonjwa mbalimbali na hasa kipindupindu.