Ijumaa , 30th Sep , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasili Dodoma muda huu, akiongozana na mke wake na kupokelewa nyumbani kwake maeneo ya Mlimwa C, mjini humo.

PICHA: Maktaba.

Katika safari hiyo Waziri Mkuu ameondoka Jijini Dar es Salaam kwa ndege ya kukodi aina ya Beach Craft 190.

Mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma, Majaliwa amepokelewa na Waziri wa ofisi ya Rais Tamisemi George Simbachawene, Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama.

Wengine waliompkea Waziri Mkuu ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana, Meya wa Manispaa ya Dodoma Jafari Mwanyemba, Mbunge wa Dodoma mjini Anthony Mavunde na wabunge wa mkoa wa Dodoma.

Wengine ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma Adam Kimbisa na wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma.

Katika mapokezi hayo, mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme amesema kuwa ujio wa Waziri Mkuu mkoani Dodoma utafungua milango ya fursa katika mkoa huo na pia umeiweka Dodoma katika ramani ya Tanzania.

Naye Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene amesema kuwa kitendo cha Waziri Mkuu Kasim Majaliwa kuhamia Dodoma ni kithibitisho kuwa tayari serikali imeshahamia Dodoma

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana ametoa ratiba ya ziara ya kesho kuwa ataenda kutembelea hospital ya rufaa ya mkoa wa Dodoma, TANESCO, visima vya kuzalishia majisafi vilivyoko Mzakwe, Mamlaka ya ustawishaji makao Mkuu CDA na sokoni.