Jumanne , 15th Mar , 2016

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,amewaonywa watendaji wa vijiji vilivyo na mipaka ya nchi jirani kuacha kuwaingiza raia wa nchi za kigeni kinyemela na kinyume cha taratibu ikiwemo kutoa vibali vya wageni hao kuishi nchini.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa

Akizungumza jana Mkoani Kagera wilayani Misenyi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Kakunyu waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, amesema kuwa kijiji hicho cha Kakunyu kimekithiri kuwaingiza wageni kutoka nchini Uganda pamoja na mifugo yao.

Waziri Mkuu majaliwa amewapiga maarufu watendaji wa Vijiji, Wenyeviti wa vijiji kutoa vibali vya wageni kuingia nchini na kusema kuwa kazi hiyo inafanywa na idara ya uhamiaji nchini.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa kamwe serikali ya awamu ya tano haitakubali ardhi yake kutumiwa kama shamba la bibi kwa wageni wakati wananchi wake wakikosa ardhi ya kufanyia shughuli zao ikiwemo kilimo na Ufugaji huku wawekezaji wakijilimbikizia ardhi bila ya kuiendeleza.

Ziara ya Waziri Mkuu inatarajiwa kuendelea leo katika wilaya ya Ngara ambapo atakagua kituo cha kupokelea wakimbizi cha Rumasi na kuzindua mradi wa uzalishaji umeme Wilayani humo.