Jumapili , 8th Oct , 2023

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amezitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Ranchi za Taifa (NARCO) na Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Mafunzo (LITA) kuwa na mkakati wa pamoja wa kuwaandaa vijana kuwa wafanyabiashara katika sekta ya mifugo kupitia programu kielelezo ya BBT Mifugo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega

Waziri Ulega ametoa maelekezo hayo wakati akizindua Bodi ya Nne ya Ushauri ya Wakala ya Mafunzo (LITA) na Bodi ya Wakurugenzi ya Ranchi za Taifa (NARCO) jijini Dar es Salaam

"Huu ndio uwe mtazamano wetu, kijana anapofundishwa na kumaliza mafunzo yake pale LITA nyie NARCO muweke utaratibu wa kutenga maeneo kwa ajili ya kuwapa vijana hao ili wajifunze kwa vitendo ufugaji wa kisasa, hatutaki kufundisha watu ili waende kuhangaika bali waingie katika biashara ya mifugo na mazao yake," amesema Waziri Ulega 

Aidha, aliwataka  LITA kuhakikisha wanakuwa na mkakati wa kuwaunganisha vijana hao na taasisi za kifedha kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kuwapa mbinu za kutekeleza mkakati wa kibiashara na kupata mitaji.

Halikadhalika, ameielekeza  NARCO kuhakikisha wanaweka mikakati ya kuvutia wawekezaji na kuhakikisha wanakuwa kinara wa biashara ya nyama nchini.