Jumamosi , 26th Dec , 2015

Wazee nchini wamemuomba Rais John Pombe Magufuli awasaidie kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo kukosa huduma bora za afya, lishe bora pamoja na kutolipwa mafao yao kwa wakati pindi wanapostaafu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, (kushoto) akizungumza na Makamu wake, Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Wakizungumza katika baraza la wazee la Kimandolu, wazee hao wakiongozwa na Amon Mwita wamesema kuwa licha ya mchango wao katika uchumi wa nchi na maendeleo ya taifa tangu kipindi cha uhuru wamekuwa ni watu wa kusahaulika jambo ambalo linawafanya waishi wa shida.

Navoneiwa Maeda ni mzee ambaye ameitaka serikali iwathamini wazee kwani ni kundi linaloishi katika mazingira magumu na bado halijapewa kipaumbele na serikali jambo ambalo linawaumiza…

Mwenyekiti wa baraza la wazee mtaa wa Kimandolu Emmanuel Mollel amesema kuwa wazee wengi wamekuwa wakijificha majumbani ingali wagonjwa bila kupata matibabu na wengine kutopata mlo wa siku kutokana na hali ngumu za kiuchumi walizonazo hivyo ameiomba jamii ijitokeze kuwasaidia wazee.

Mkurugenzi wa Jamii Media Group Pamela Mollel na Mdau wa wazee Amedeus Moshi waliofika kuwatembelea wazee hao na kutoa msaada wa kibinadamu wameitaka jamii itambue wajibu wake wa kuwalinda na kuwatunza wazee pamoja na kukemea mauaji ya vikongwe suala linalochafua taswira ya taifa na kuathiri ustawi wa wazee nchini.

Wazee nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa huduma za afya, chakula ,malazi duni na mahitaji muhimu ya kibinadamu suala ambalo linachangia msongo wa mawazo miongoni mwa wazee wengi na kujikuta wakitumbukia katika ulevi wa kupindukia hivyo jamii na serikali haina budi kuwasaidia wazee.