Jumanne , 6th Oct , 2020

Watu wawili wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kwa kosa la wizi wa pesa na simu vyenye thamani ya shilingi za kitanzania zaidi ya Laki nne.

Picha ya pingu

Watu hao ni Rajabu Hassan na Lukmani Juma ambao wamesomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Happiness Kikoga na Wakili wa serikali Hamisi Saidi.

Washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo tarehe 20, Julai 2020, katika eneo la Kinondoni ambapo waliiba simu aina ya TECNO POP 1, yenye thamani ya shilingi laki mbili pamoja na fedha za kitanzania kiasi cha shillingi laki mbili na ishirini mali ya Yuweni Jackson, ambapo baada ya kupokonya mali hizo washtakiwa walimjeruhi kwa silaha aina ya Panga.

Baada ya kusomewa shtaka hilo washtakiwa wamekana kutenda kosa hilo na Hakimu Kikoga ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba, 19 mwaka huu na kudai kuwa dhamana kwa washtakiwa imefungwa kwa mujibu wa sheria.