Jumapili , 28th Feb , 2016

LICHA ya kuwekwa kwa zuio la shughuli za uvuvi katika ziwa Rukwa kufuatia kufungwa kwa ziwa hilo kwa muda,imebainika kuwa baadhi ya wavuvi wanakaidi agizo hilo na kuendelea na shughuli hizo kama kawaida ndani ya ziwa hilo.

Wavuvi wakiwa katika harakati za kusaka Samaki

Mkuu wa wilaya ya Momba mkoani Songwe Richard Nambeho,amesema wapo wavuvi wanaoendelea na shughuli za uvuvi ndani ya ziwa Rukwa jambo linalokiuka sheria iliyowekwa na kutekelezwa na halmashauri za wilaya zote zinazozunguka ziwa hilo.

Katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Momba,mkuu wa wilaya huyo amevilalamikia vyombo vya ulinzi na usalama akisema havilifanyii kazi agizo la kufungwa kwa muda ziwa hilo na ndiyo sababu baadhi ya wavuvi wasio watii wanaendelea kufanya shughuli zao.

Nambeho pia amelalamikia Ofisi ya idara inayohusika na Uvuvi akisema inashiriki katika ukaidi huo kwakuwa inasemekana wapo wavuvi ambao wamekatiwa vibali vya kufanya shughuli zao ndani ya ziwa hilo katika kipindi hiki ambacho shughuli zote zimesimamishwa.

Amesema pia dhambi ya ukiukaji agizo la kufungwa kwa ziwa hilo haiwezi kumkwepa Afisa Tarafa ya Kamsamba na viongozi wengine waliopo kwenye tarafa hiyo kwakuwa hawatoi ushirikiano kwenye zoezi la zuio la shughuli za uvuvi ndani ya ziwa Rukwa.

Mkuu huyo wa wilaya amemuagiza afisa tarafa ya Kamsamba kuwasilisha mpango kazi wa namna gani ofisi yake imejiandaa kupambana na watu wanaokiuka agizo la kufungwa kwa ziwa hilo iwapo kweli ana nia ya dhati ya kushirikiana na serikali wilayani humo.

Amewataka pia madiwani wa kata zilizopo jirani na ziwa Rukwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya watu wanaokiuka agizo la kufungwa kwa ziwa hilo kwakuwa nia ya serikali ni njema kwa kila mmoja anayeweza kunufaika na shughuli za ziwa hilo.