Alhamisi , 28th Sep , 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amewataka watumishi wa umma kuwa tayari kufanya kazi sehemu yoyote watakayopangiwa kwani utumishi wa umma ni utayari wa kukubali kufanya kazi mahali popote.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete

Kikwete ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, ikiwa ni ziara yake ya kimkakati ya kusikiliza na kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili Watumishi hao ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Amesema Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora imekuwa ikipokea maombi kutoka kwa wazazi wakiomba kuwabadilishia watoto wao vituo vya kazi pindi wanapopangiwa mikoa ya pembezoni, wakiomba wapangiwe mijini hususani Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza.

Amewasihi wazazi hao kuwaacha watoto wao wakafanye kazi katika vituo walivyopangiwa kwani katika mikoa hiyo ya pembezoni wanaoishi pia ni Watanzania sawa na wale wanaoishi mijini na kwamba nao pia wanahitaji kuhudumiwa kama wengine.

"Watumishi wenzangu hakuna watumishi ambao ni maalum kwa ajili ya kufanya kazi mikoa ya pembezoni hivyo nawasihi mtulie kwenye vituo vya kazi mlivyopangiwa na kuendelea kuwahudumia wananchi," Mhe. Kikwete amesisitiza.