Jumatano , 9th Nov , 2016

Wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nchini China wameshauriwa kuzingatia viwango vya ubora kwenye bidhaa zinazohitaji ubora sambamba na kufanyabiashara kwa kufuata mifumo ya halali ili kukwepa hasara zinazoweza kujitokeza.

Bandarini Dar es Salaam

Akiongea na East Afrika Radio katika mahojiano maalum juu ya hali ya kibiashara katika bandari ya Dar es salaam, Mwenyekiti wa kampuni ya JAVIS International Trade, Bw. Harun Marwa amesema kwa sasa ugumu katika bandari ya Dar es salaam, inatokana na wafanyabiashara kutotambua ni viwango gani ambavyo shirika la Viwango Tanzania TBS, linavihitaji hali ambayo husababisha hasara kubwa pale bidhaa inaposhindwa kutumika nchini.

Marwa, ameongeza kuwa bado suala la ushuru kupanda bila utarartibu linaendelea, huku ucheleweshaji wa mizigo nao ukiendelea jambo ambalo amedai linasababishwa na utendaji kazi usio wa ufanisi wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA bandarini hapo.

Naye Bwana Leon John ambaye ni meneja wa tawi la China wa Javis International Trade amewata wafanyabiashara, kununua bidhaa kutoka kwa wauzaji wakuu na watengenezaji wakubwa nchini China ili kupata bidhaa zenye ubora, na kuachana na kuchukua bidhaa madukani jambo ambalo linachangia kununua bidhaa isiyo na ubora na kusababisha hasara.