Kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha Libaratusi Sabasi
Jeshi la pilisi mkoani Arusha limetaja majina ya watuhumiwa 19 wanaodaiwa kuwa ndio vinara wa mtandao wa matukio yote ya milipuko ya mabomu na umwagaji wa tindikali yaliyotokea katika maeneo mbali mbali ya mkoa wa Arusha
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha Libaratusi Sabasi amewataja baadhi ya watuhumiwa wanaodaiwa kushiriki kwa namna moja ama nyingine katika matukio yote yaliyowahi kutokea Arusha kuwa ni pamoja na Jafari Lema , Yusuph Husein, Abdul Mohamed na Yahaya Hasani Hela anayedaiwa kuwa kiongozi mkuu wa mtandao huo ambaye bado anatafutwa.
Kamanda Sabasi amesema watuhumiwa wote 19 ambao wanatarajiwa kufikishwa mahakaman wakati wowote kuanzia sasa wamebainika kuhusika na ugaid huo tangu tukio la kwanza la mlipuko uliotokea nyumbani kwa aliyekuwa katibu wa bakwata mkoa wa Arusha Abraham Jonjo lililotokea tarehe 25 /10/2012 , mlipuko wa bomu kwenye kanisa la Olasiti tarehe 05/05/2013 , na mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa CHADEMA uliotokea viwanja vya soweto tarehe 15/06/2013.
Kwa mujibu wa kamanda Sabas watuhumiwa wote 19 wanahusishwa kwa namna moja ama nyingine na matukio ya milipuko katika baa ya Arusha Night Pack,tarehe 13/04/2014 , mlipuko katika mgahawa wa Vama na matukio ya umwagaji wa tindikali kwa viongozi wa dini yaliyotokea katika maeneo mbalimbali
Aidha kamanda Sabasi ameendelea kuwaomba wananchi kuacha kuwafumbia macho wahalifu kwani mhalifu hana tija kwa namna yeyote hata kama ni ndugu mtoto ama mzazi wako na amekumbusha kuwa yeyote anayemuhifadhi mhalifu akibainika, naye ni muhalifu kwa mujibu wa sheria
Kamanda Sabas amesema donge nono ambalo hakulitaja litatolewa kwa atakayewezesha kukamatwa kwa Yahaya Hassan Hela anayedaiwa kuwa kiongozi wa mtandao huo