Jumanne , 26th Jan , 2016

WATOTO wawili wamefariki dunia baada ya kuzama katika shimo la maji ya mvua lililokuwa limechimbwa kwa ajili ya matumizi ya choo huku mwingine akikutwa amefariki ndani ya shimo la kuhifadhia maji ya mvua.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga Mihayo Msikhela.

Akithibitisha kutokea kwa matukio hayo kamanda wa polisi mkoa wa Tanga Mihayo Msikhela amesema kuwa tukio la kwanza limetokea kijiji cha Kwemigole kata ya kwedibungo wilayani Kilindi mkoani Tanga.

Amesema mtoto huyo mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili aitwaye Mwajuma Iddy alizama katika shimo hilo na kupelekea kifo chake papo hapo na kuwa upelelezi unaendelea kuhusiana na tukio hilo.

Katika tukio la pili mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 6 aliyefahamika kwa jina la Bakary Mwapi alikutwa na baba yake mzazi Mwapi Lugendo (32) mkazi wa Mgera akiwa amefariki dunia ndani ya shimo la maji ya mvua linalotumiwa kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya kufyatulia matofali.

Kamanda Msikhela amesema jeshi la polisi linaendelea kufanya upelelezi ili kubaini chanzo kilichopelekea kifo cha mtoto huyo.

Katika matukio mengine Kamanda Msikhela amesema mtu mmoja mkazi wa Mtimbwani Wilayani Mkinga aitwaye Tuwa Mbwana (38 ) mkulima amefariki dunia baada ya kujinyonga katika chumba anacholala.

Alisema marehemu alijinyonga kwa kutumia kamba ya manila na kufariki papo hapo na kueleza kuwa marehemu hakuwa na ugomvi na mtu yeyote na mwili umefanyiwa uchunguzi wa kitaalamu na daktari na kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.

Wakati huo huo mtu mmoja aitwaye Prima Dominika (43) mkazi wa Mikanjuni Boznia kata ya Ngamiani Kati jijini Tanga nyumba yake yenye vyumba 7 iliungua moto na kuteketeza vyumba 4 vilivyopo katika nyumba hiyo.

Alisema thamani ya vitu haijafahamika na chanzo cha moto huo ni kutokana na mtoto aitwaye Jephason Prima mwenye umri wa miaka 6 ambaye alikuwa akichezea kiberiti kwa kuwasha baadhi ya vitu vilivyopo ndani ya chumba anacholala na kupelekea kuanza kwa moto huo.