Jumatatu , 28th Dec , 2015

Katika hali isiyokuwa ya kawaida vitendo vya unyanyasaji kwa watoto hapa nchini bado vinazidi kushika kasi katika maeneo mbalimbli hapa nchini na kusababisha ulemavu,mateso na hata vifo.

Watoto wawili Asha Ramadhani (4) na Ismail Ramadhani (5) wamechomwa moto na mtu anaedaiwa kuwa ni shangazi yao katika kitongoji cha Stooni, kata ya Nakatungulu, mjini Nansio wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea hivi majuzi ambapo watoto hao walichomwa viganja vya mikono na shangazi yao Ashura Ismail (30) kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni kuiba kitoweo.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Ukerewe, Ally Mkalipa amethibitisha kuwapo tukio hilo ambalo mtuhumiwa ni Ashura Ismail na kuongeza kuwa uchunguzi umekamilika na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote.

“Ni kweli tumepokea malalamiko hayo na baada ya kumhoji mtuhumiwa amekiri kutenda kosa kwa kile alichodai kupatwa na hasira baada ya watoto hao kukaidi mara kwa mara maelekezo yake,” alisema Mkalipa.

Shangazi wa watoto hao, akijitetea, alidai watoto hao waliokuwa wakiishi na baba yao katika kambi za uvuvi, ni watukutu na kwamba wakionywa hawatii. Alidai, kwa muda mrefu kaka yake ambaye ni baba wa watoto hao aliwatelekeza nyumbani kwake bila ya kutoa msaada wa aina yoyote.

Kwa upande wao watoto hao walidai mbali ya kupewa adhabu hiyo ya kuchomwa moto viganja vya mikono, pia walikuwa wakipigwa mara kwa mara na kunyimwa chakula na baada ya watoto hao kupelekwa hospitali uchunguzi wa kitabibu ulibaini licha ya majeraha ya moto waliyo nayo, wanakabiliwa na magonjwa ya homa ya tumbo, malaria na utapiamlo.

Kutokana na hali ya miili ya watoto hao kudhoofu kwa sasa wanalelewa na mtetezi wa masuala ya kibinadamu Bwn Daniel Kondayo wakiendelea kupatiwa tiba pamoja na lishe ili waweze kupata afya bora.