Alhamisi , 14th Mei , 2020

Watoto wadogo wanaosoma Darasa la Nne na la Pili, huko Mkoani Geita, ambao taarifa zao za kudaiwa kufunga ndoa zilisambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, wamesema kuwa hiyo haikuwa ndoa halisi na kwamba walifanya tu kama mchezo wa kitoto.

Watoto wa Darasa la 2 na 4, wanaodaiwa kuoana huko mkoani Geita.

Hayo wameyabainisha walipozungumza na EATV kwa nyakati tofauti na kueleza kuwa hiyo ilikuwa tu ni sherehe ya kitoto na kwamba walipikiwa wali na maharage.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, amesema kuwa tukio hilo limetokea Mei 11, na kwamba idadi ya watoto waliohudhuria ilikuwa ni kubwa zaidi ukilinganisha na idadi ya watu wazima, huku ikidaiwa kuwa hata wazazi wa watoto hao hawakuwepo eneo la tukio, licha ya uwepo wa chakula.

"Kwa harakaharaka tunaweza tukasema kuwamba zilikuwa ni shughuli za watoto zilizokuwa zinafanyika hapo mtaani, tumefuatilia na bado tunafuatilia ili kuona wahusika halisi wa tukio hilo, kuna mambo ya msingi tunataka kuona ikiwemo suala la chakula, lakini pia tunataka tuone kama kweli lilikuwa ni suala la watoto au kulikuwa na umakini ndani yake" amesema Kamanda Mponjoli.