Ijumaa , 24th Jun , 2016

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, TAMWA, kimeitaka serikali kuhakikisha inapitia upya hatua inazochukua kupambana na ukatili wa kingono dhidi ya watoto na ndoa za utotoni ambazo zinazidi kuongezeka nchini.

Eda Sanga Mkurugenzi wa TAMWA akiongea na waandishi wa habari

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa TAMWA, Bi. Eda Sanga  jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza kwenye semina ya  waandishi wa habari kuhusu kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ndani ya jamii dhidi ya wanawake na watoto.

Bi.Eda Sanga amesema, kwa sasa idadi ya watoto wanaopata ujauzito katika umri mdogo na kukatishwa masomo inaongezeka siku hadi siku jambo linalotishia ustawi wa jamii kwani wanapokatishwa masomo ndio chanzo cha ukatili kwa watoto wanaowazaa.

"Ukatili wa watoto utaishaje, endapo mtoto akimzaa mtoto hii ina maana ugumu wa maisha, changamoto zote za kiuchumi ya jinsi ya kumlea mtoto mwenzake anazikabili na umasikini ukimzunguka je nilini ukatili kwa watoto utaisha au umasikini utapotea," alihoji Eda Sanga

Akiongelea suala la ukatili wa kingono kwa watoto, Bi Eda amesema wazazi wahakikishe wanakuwa karibu na watoto wao pamoja na kuepuka watoto kusoma umbali mrefu na nyumbani.