
Mradi huo umezinduliwa katika kijiji cha Zenith ya Kati, wilayani Muheza mkoani Tanga ukiwa ni sehemu ya mradi mkubwa wa miaka mitano wa majaribio duniani chini ya Global Learning Xprize wenye lengo la kutatua matatizo ya kujifunza.
Mpango huo utagusa watoto 2,400 wa miaka kuanzia 9 hadi 11 kutoka katika vijiji 167 vya wilaya za Handeni, Korogwe, Lushoto, Muheza, Mkinga na Pangani. Timu ya wabunifu itahakikisha inawawezesha watoto waliokosa elimu ya darasani kujifunza stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa kutumia Tableti.
Mradi huo hapa nchini unaendeshwa kwa pamoja na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na XPrize ambao wametoa tableti husika.
Mwakilishi wa UNESCO anayesimamia mradi huo Faith Shayo amesema mradi huo umewezekana kuwepo kutokana na makubaliano kati ya serikali ya Tanzania kupitia Wizara yake ya elimu na TAMISEMI na mashirika husika.