Alhamisi , 20th Nov , 2014

Takwimu zinaonesha kwamba watoto 130,000 nchini Tanzania wana maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) Huku kati ya hao 39317 wamefikiwa na kupatiwa huduma ya dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Pindi Chana.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Pindi Chana wakati akifungua kongamano la Nne la kitaifa la VVU na UKIMWI kwa watoto linalofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere uliopo jijini Dar-es-salaam.

Dkt . Chana alisema asilimia 39 ya watoto walio katika hatari ya kupata maambukizi ya UKIMWI hupimwa vipimo vya kubaini maambukizi ya VVU ndani ya miezi miwili baada ya kuzaliwa hivyo basi kuna umuhimu kwa watoto hawa kupata huduma za tiba mapema.

Akizungumzia maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto waziri huyo alisema Tanzania imepiga hatua katika kuzuia maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto lengo likiwa ni kutokomeza kabisa maambukizi mapya kwa watoto wachanga.