Jumatano , 21st Sep , 2022

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka watendaji wote Serikalini kuweka mkakati wa kudhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu Majaliwa amesema lengo la agizo ni kusisitiza utekelezwaji wa maono na dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa katika hali ya utulivu ili kuendelea kufikisha maendeleo katika kila eneo.

Amesema hayo leo Jumatano, Septemba 21, 2022 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani yayofanyika katika ukumbi ya Kuringe, Moshi Kilimanjaro.

“Hatuna budi kuitunza amani yetu kulingana na umuhimu wake kwani amani ni tunda la upendo, utulivu, mshikamano na maridhiano.” -Amesema Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu 

Waziri Mkuu amesema kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa katika kutafuta na kudumisha amani na usalama kwani kila palipo na amani, shughuli za kiuchumi na kijamii hufanyika kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi kwa ujumla.

“Niwasihi wananchi kuendelea kutunza na kuilinda tunu ya amani tuliyojaliwa hapa nchini kwani jukumu la kuilinda amani hii ni agenda yetu sote, tuitekeleze.”- Amesema Kassim Majaliwa Waziri Mkuu

Pia, Majaliwa amesema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itaendelea kuchukua hatua na tahadhari zote zinazohitajika ili kuendelea kudumisha amani nchini.