Ijumaa , 17th Jun , 2016

Wananchi wanaokwenda kununua vitoweo jamii ya kuku na bata katika soko la Kawe jijini Dar es Salaam, hulazimika kuondoka sokoni hapo wakiwa wamebeba wanyama hao huku wakiwa hai, na kwenda kutafuta huduma ya uchinjaji katika maeneo wanayoishi.

Hali hiyo inatokana na kukosekana kwa huduma ya uchinjaji mifugo sokoni hapo, kama anavyoeleza mkazi wa Kawe Bw. Omary Ally Salehe ambaye baada ya kununua kitoweo chake amelazimika kwenda kutafuta huduma ya uchinjaji mahali kusikojulikana.

“Wateja tumekuwa tukipata usumbufu sana kutokana na ukosefu wa machinjio hapa sokoni...kwa mfano mimi hapa nimeshanunua kuku wangu lakini tofauti na kwenye masoko mengine, hapa nalazimika kuondoka na kuku wangu kwenda kutafuta mchinjaji huko mtaani ninakoishi,” amesema Omary.

Ameongeza kuwa kitendo cha kubeba kuku na kwenda naye nyumbani akiwa mzima ni hatari kwani anaweza kukuponyoka na kukimbia halafu ikawa hasara kwako au hata ukashambuliwa na watu kwa kudhaniwa kuwa ni mwizi wa kuku.

Yusuph Abdallah ni Mwenyekiti wa Soko hilo ambaye ameiambia EATV kwamba kwa ujumla biashara ya kuku imedorora sokoni hapo, licha ya kuwepo kwa taarifa za kutengwa fedha za ujenzi wa machinjio hayo ambayo hata hivyo hatma yake bado haieleweki.

“Mimi kama kiongozi wa soko moja ya malalamiko ninayoyapata ni kutoka kwa wafanyabiashara wa kuku...wamekuwa wakilalamikia kudorora kwa biashara kunakotokana na ukosefu wa machinjio..siku hizi watu hawana utamaduni wa kuchinja wenye kwa hiyo wanategemea huduma yote hiyo ipatikane kwa muuzaji,” amesema Bw. Yusuph.

Ametaja moja ya hatua alizochukua ni kwa kuwasilisha maombi kwa uongozi wa Manispaa ya Kinondoni na kwa mujibu wa bajeti ya Manispaa kwa mwaka unaoishia Juni mwaka huu, soko la Kawe lilitengewa zaidi ya shilingi milioni hamsini kwa ajili ya ujenzi wa machinjio.

“Lakini cha ajabu kumekuwa na dana dana mpaka sasa hakuna dalili za kuanza kwa ujenzi na isitoshe hatujui kama hizo fedha tutazipata kweli au ni danganya toto kwani mwaka wa fedha ndiyo unaenda ukingoni na hatujui kama hizo pesa zitatengwa katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha,” amefafanua Mwenyekiti huyo wa Soko la Kawe.