Chanzo cha Maji
Rai hiyo imetolewa jana Agosti 15 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi, Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu wakati wa ziara ya Bodi hiyo pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) walipotembelea miradi ya waendelezaji binafsi wa umeme iliyowezeshwa na REA katika Mkoa wa Njombe.
Wakati wa ziara hiyo, Wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti waliweza kutembelea mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji wa Lupali uliopo kijiji cha Boimanda Wilaya ya Njombe ambao kukamilika kwake mradi huo utaweza kuzalisha Kilowati 317 (kW) pamoja na mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji wa Lupendo ambao uzalisha Megawati 2.9
“Tumekuwa na muendelezo wa ziara za Bodi pamoja na Menejimenti kutembelea miradi ya waendelezaji binafsi wa umeme katika Mkoa wa Njombe na leo tumetembelea miradi miwili ambayo pamoja na wadau wengine, REA ina mchango mkubwa katika miradi hiyo.
Serikali kupitia REA imetoa fedha nyingi sana kuwezesha miradi hii kukamilika ili kuendelea kuongeza uhakika wa umeme kwa ajili ya kuwaletea maendeleo mwananchi mmojammoja na Taifa kwa ujumla. Ili miradi hii iwe endelevu tunaendelea kuwasisitiza wananchi kutunza mazingira tuendelee kuwa na maji ya uhakika kuendesha mitambo na hivyo kuwa na umeme wa uhakika pia,” amesisitiza Mwenyekiti Kingu.
Kwa upande wake msimamizi wa mradi wa Lupali ambao unaendeshwa na shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha, Sister Imakulata Mlowe ameishukuru REA kwa ufadhili walioutoa kuwezesha mradi huo ambapo REA imechangia asilimia 77 ya gharama za ujenzi wa mradi huo ambao unagharimu Zaidi ya Shilingi Bilioni 6.
Naye Meneja Mkuu na Mkurugenzi wa Rift Valley Energy, Deo Massawe amesema kuwa tangu kuanza kwa mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji wa Luponde wameweza kuunganisha wananchi, shule, hospitali pamoja na viwanda vya chai.