Alhamisi , 18th Sep , 2014

Watanzania wametakiwa kuungana kuwafichua watu wanojihusisha na vitendo vya ukatili ikiwemo kuwakata viungo na kuwauwa watu wenye ulemavu wa ngozi maarufu kama albino.

Afisa Uendeshaji wa Taasisi ya Under The Same Sun Gamariel Mboya (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa taasisi hiyo Bi. Vicky Ntetema.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) Bi. Marry Massay, amesema hayo leo wakati akizungumzia maandamano ya amani kupinga vitendo vya ukatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, maandamano yaliyoandaliwa ofisi yake kwa kushirikiana na Chama cha Albino Tanzania na taasisi ya Under the Same Sun.

Bi Massay amesema haiwezekani kuona vitendo vya ukatili dhidi ya albino vikiendelea pasipo wahusika kukamatwa kwani wanaopanga na kutekeleza ukatili huo wanafahamika kwani ni sehemu ya watu tunaoishi nao katika jamii.

Awali, Afisa Uendeshaji wa taasisi ya Under The Same Sun, Gamariel Mboya, amesema watu wenye ulemavu wa ngozi wamekuwa katika hatari kubwa ya kushambuliwa kutoka kwa watu wenye imani tofauti na kwamba kuna haja ya kuunganisha nguvu kupambana na vitendo hivyo.