Jumatatu , 14th Apr , 2025

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro ametoa rai kwa Watanzania wote kuwapuuza wanasiasa wanaowashawishi kutoshiriki katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro

Ndumbaro ametoa rai hiyo leo katika uwanja wa Mashujaa manispaa ya Bukoba wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani Kagera.

"Katiba yetu iko wazi kabisa, vigezo ambavyo vitamzuia mtu kutoshiriki uchaguzi ni endapo sio Mtanzania, au ana matatizo ya akili, ni mhalifu aliyetiwa hatiani na ambaye hana kitambulisho cha mpigakura, sasa kama Mtanzania hauna kasoro hizo kwanini usitumie haki yako kikatiba kushiriki uchaguzi ", amesisitiza Dkt Ndumbaro 

Dkt Ndumbaro ameongeza kuwa wapo wanasiasa ambao wamekuwa wakipotosha juu ya  Haki za Binadamu wakijikita katika haki za kisiasa pekee wanasahau kumpongeza Mheshimiwa Rais anaayetekeleza haki kwa watanzania katika nyanja mbalimbali kama vile ujenzi wa miundombinu inayowezesha kuboresha maisha na kuleta maendeleo.

Aidha Dkt Ndumbaro ametoa wito kwa viongozi wa dini kukemea maovu hasa kwa wale wanaojichukulia Sheria mkononi na kugeuka chanzo cha migogoro pia familia zijikite katika kutafuta mapatano na sio kuongeza migogoro  hususan ya ardhi na mirathi.