Jumatatu , 24th Aug , 2015

Wanawake wanaowania uongozi katika nafasi ya udiwani wa kata na viti maalum katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma wametakiwa kujiamini na kujitokeza katika kuwania nafasi hizo kwa kuwa wanaweza.

Mmmoja wa Wanawake akiwa katika mdahalo wa kuelemisha juu ya Uongozi katika Kijiji

Wito huo umetolewa jana na meneja program wa haki za jinsia kutoka shirika lisilo la kiserikali la Oxfam, Rashida Shariff wakati akizungumza kwenye semina ya kuwajengea uwezo wanawake wanaowania nafasi ya uongozi ngazi ya udiwani katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino.

Amesema kuwa shirika hilo limehakikisha kuwa wanawake wanaweza kushiriki wanavyoweza katika uchaguzi wa mwaka huu kama viongozi, kwa kuwa wanawake wengi wako nyuma kushiriki katika uchaguzi kama wagombea lakini mara nyingi hushiriki kama wapiga kura.

Kwa upande wake mratibu wa mradi wa Fahamu, Ongea, Sikilizwa kutoka shirika lisilo la kiserikali la Woman Wake Up (Wowap), Nasra Suleiman amesema kuwa mradi huo unatekelezwa katika wilaya za Mpwapwa na Chamwino mkoani Dodoma kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanawake ambao wanagombea udiwani katika wilaya hizo kwa vyama mbalimbali za kisiasa.