Wanawake mkoani Shinyanga
Wakizungumza wanawake wa Manispaa ya Shinyanga wamesema changamoto kubwa ni mikopo umiza wanayochukua mitaani ambayo inasababisha wanawake wengi kuuziwa vitu vya ndani na ndoa zao kuwa hatarini.
Akizungumza baada ya kutembelea baadhi ya shule za sekondari kisha kuzungumza na makundi mbalimbali ya kijamii, Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Shinyanga Salome Makamba amesema mikopo umiza imekuwa ni janga kubwa kwa jamii.
Mariam Senkondo mkazi wa Manispaa ya Shinyanga amesema mikopo umiza imekuwa ni janga kubwa kwa wanawake kutokana na wanawake wengi kukimbilia mikopo hiyo kwa kuwa masharti yake ni nafuu na matokeo yake wengine wanakimbia familia.
"Jamani wakina mama tuna wakati mgumu sana, tunapenda mikopo ili tufanye biashara itusaidie lakini tunaumizwa na mikopo umiza wengine wanaita kausha damu ukisema uende benki masharti ni magumu ndiyo maana wengi wanaishia mikopo umiza," amesema Vumilia.
Aidha wanawake hao wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwadhibiti watu wanaofanya biashara ya kukopesha fedha na kutoza riba kubwa ambayo imekuwa kama njia ya kuwakandamiza wenye kipato cha chini.