Jumatano , 13th Dec , 2017

Wimbi la kuhama vyama kwa wanasiasa nchini limewachanganya wananchi kiasi cha kushindwa kutambua Chama kipi kinafaa ama kiongozi gani mwenye msimamo kisiasa.

''Siasa imekuwa na mihemko kwa kipindi hiki vuguvugu linaendelea, hii inasababisha sisi kutoelewa kuwa upinzani au chama tawala yupi yupo sahihi, maana yule aliyekataliwa CCM siku hizi anakubalika upinzani na aliye kataliwa upinzani anakubalika Chama tawala'', amesema mfanyabiashara wa bidhaa ndogondogo Kelvin John Mjema.

Hayo yamebainishwa na wananchi tofauti katika soko la Mwenge wakati wakizungumza na East Africa Television.
Naye Aisha Ramadhani Mama Ntilie katika eneo la Mwenge amefunguka na kusema yeye kwasasa vyama vimemtibua na hataki kabisa kushabikia chama chochote.

"Sihitaji kushabikia mtu kwasasa, maana unashabikia mtu na chama fulani ghafla siku mbili unamuona kaondoka kaenda chama kingine, na wewe unahama, ukifika huko baada ya muda naye anahama sasa unashindwa kufahamu ufanye nini, kwakweli CUF, CCM na CHADEMA wanatuchanganya sana kwasasa", amesema Aisha.

Kumekuwa na wimbi kubwa la viongozi wa siasa kuhama vyama vyao huku wakisababisha majimbo waliyoyaacha wazi kuandaliwa uchaguzi na NEC ambao hugharimu zaidi ya  shilingi milioni 80.

Miongoni mwa majina makubwa ambayo  yamehama vyama siku za hivi karibuni ni pamoja na aliyekuwa Mbunge  wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu kuhamia CHADEMA aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni kupitia CUF Maulid  Mtulia kuhamia CCM pamoja na makada wengine mbalimbali.