Ijumaa , 18th Sep , 2015

Wamiliki wa mitandao ya mawasiliano nchini wametakiwa kutoa taarifa haraka juu ya makosa ya uharifu wa mitandaoni pindi yanapojitokeza, ili kuvirahisishia vyombo vya usalama kuweza kuchukua hatua za haraka kwa wahusika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Patrick Makungu akifafanua jambo

Wito huo umetolewa leo mkoani Mtwara na mkuu wa upelelezi wa polisi wilaya ya Masasi, SP Nathaniel Kyando, wakati wa semina ya mahakimu, waendesha mashitaka na wapelelezi kuhusu elimu ya sheria ya makosa ya mtandao na sheria ya miamala ya kielektroniki ya mwaka 2015.

Kwa upande wake, mkuu wa kitengo cha sheria kutoka Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Veronica Sudayi, akizungumza kwa niaba ya katibu mkuu wa wizara hiyo, amesema jamii inatakiwa kufahamu kwamba sheria hiyo haina vitu vipya isipokuwa ni mabadiliko ya kimfumo ambayo yameingiza makosa hayo katika mfumo wa kielektroniki.

Aidha, mwanasheria kutoka wizara hiyo, Anna Kalamo, amesema miongoni mwa mada ambazo wanapatiwa wahusika ni pamoja na sheria mbili ambazo zimepitishwa na serikali za miamala ya kielektroniki na sheria ya makosa ya mitandao zote za mwaka 2015 ambazo zimetungwa kwa lengo la kuleta ulinzi na matumizi salama ya mitandao hapa nchini.