Wakazi zaidi ta 350 wa vijiji vitatu vilivyopo kata ya Maere jijini Tanga wamelalamikia zoezi la kujiandikisha katika daftari la wapiga kura kufuatia kituo walichozoea kujiandikisha katika chaguzi mbalimbali zilizopita kuhamishiwa umbali wa kilomita Saba kutoka katika makazi yao hatua ambayo inawalazimu baadhi ya wasamaria wema kujitolea kukodisha usafiri wa pikipiki almaarufu boda boda kuwapeleka watu kwa awamu ili waweze kufanikisha zoezi hilo.
Wakizungumza katika maeneo tofauti yaliyopo kata ya Maere jijini Tanga wakazi hao wamelalamikia kitendo hicho kufuatia mwandikishaji kulazimishwa kukataa kwenda katika makazi ya watu na badala yake wameweka kituo hicho umbali mrefu na makazi ya watu hivyo wameiomba tume ya taifa ya uchaguzi jimbo la Tanga kurekebisha kasoro hizo mapema kabla ya siku ya mwisho ya uandikishaji haijawadia ili waweze kutumia haki yao ya msingi ya kujiandikisha ili waweze kuchagua viongozi wanaowataka.
EATV imetembelea katika kituo hicho kinacholalamikiwa kuwa mbali na makazi ya watu ambapo hakuna mtu hata mmoja aliyekutwa akijiandikisha katika zoezi hilo na badala yake walikutwa watoto wakiwa na mwandikishaji Mariam Issa ambaye alikiri kuwepo kwa uhaba wa watu kujitokeza kufuatia tangu kuanza kwa zoezi hilo jumla ya watu 120 ndiyo waliojiandikisha kati ya watu zaidi ya 500 waliopo katika mitaa aliyopangiwa kufanya kazi .
Baadhi ya wagombea nafasi katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika katikati ya mwezi ujao wameiomba tume ya taifa ya uchaguzi jimbo la tanga kuharakisha kufanya marekebisho hayo ili kuepuka migogoro ya kisiasa inayoweza kujitokeza katika maeneo hayo