Alhamisi , 11th Jul , 2024

 Licha ya serikali kufanya jitihada za ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule zilizopo kata ya ihanamilo eneo hilo linakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji jambo ambalo linasababisha wanafunzi kushindwa kufanya usafi wa vyoo kwa wakati na kuwaweka hatarini kupata ma-gojwa ya mlipuko.

Simoni Shija-Afisa Elimu kata ya Ihanamilo

Hayo yamebainishwa na Afisa elimu kata ya Ihanamilo Simoni Shija Pamoja na diwani wa Kata hiyo Joseph Rugahila wakati wa ziara ya Mbunge wa jimbo la Geita mjini Costantine Kanyasu alipotembelea katika shule ya msingi Ikulwa kukagua ujenzi wa matundu 17 ya vyoo unaoendelea katika eneo hilo.

Changamoto ya maji katika kata hiyo haiathiri taasisi peke yake bali hata wananchi wa kawaida.

 “Wake zetu wakienda kuchota maji wanasubiria sana ili wengine wachote maana watu ni wengi na unakuta wanamaliza muda mrefu bila kupata maji jambo ambalo linasababisha migogoro ya ndoa katika miji yetu tunaomba serikali ituletee maji tuokoe ndoa zetu”Butimanye Malagilo, Mkazi wa Nyakahengere
 
Mbunge wa jimbo la Geita Mjini Costantine Kanyasu anakiri kuwa kuna shida ya maji lakini anaeleza kuwa kuna mradi mkubwa wa maji unakuja umaotarajiwa kutatua changamoto hiyo.