
Kikosi cha uokoaji kikiendelea na zoezi la kufukua kifusi katika choo kilichotitia, shule ya msingi Siliani.
Akizungumza na www.eatv.tv, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru iliyopo mkoani humo, Jerry Murro amesema kuwa tukio hilo limetokea asubuhi majira ya saa 4, ambapo mwanafunzi mmoja amejeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya wilaya.
Muro amewataka wananchi kuwa watulivu wakati wa zoezi la ufukuaji wa vifusi vilivyoporomoka katika choo hicho ili waweze kuona kama kuna wanafunzi wengine wamefukiwa ingawa inasemekana walikuwa zaidi ya mmoja ndani ya choo hicho.
"Tayari kikosi cha uokoaji kinaendelea na kazi ya kutoa vifusi ili kuangalia kama kuna wanafunzi wengine waliofukiwa, na baadaye tutaunda tume ya uchunguzi wa tukio hili ili kufahamu chanzo", amesema Muro.
Kutokana na shule hiyo kuwa na choo kimoja chenye matundu ishirini ambacho ndicho kilikuwa pekee kwa shule hiyo, imemlazimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru kuchukua hatua za kuzungumza na uongozi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Seliani na kuomba shule kutumia vyoo vya Kanisani hilo, ombi ambalo lilikubaliwa na Mkuu wa jimbo la Arusha Magharibi, Mchungaji Philemon Joseph Mollel ambae aliungana na Mkuu wa Wilaya katika zoezi la uokoaji na hivyo kuondoa mashaka ya kufungwa kwa shule hiyo.