Alhamisi , 9th Mei , 2024

Baada ya tukio la mtoto wa miaka 10 mwenye ulemavu wa ngozi mkazi wa Mtakuja kata ya Katoro wilayani Geita kushambuliwa kwa panga na kujeruhiwa sehemu za kichwani na mkononi, Umoja wa Waganga na Wakunga wa Tiba Asili Tanzania UWAWATA umelaani vikali tukio hilo.

Bujukano Mahungu John, Mwenyekiti wa Umoja wa Waganga na Wakunga wa Tiba Asili Tanzania

Mwenyekiti wa UWAWATA, Bujukano Mahungu John akiwa katika kitongoji cha Busambilo Kata ya Minkoto wilaya ya Chato mkoani Geita amekemea vikali tukio hilo huku akiliomba jeshi la polisi kuendelea kufanya uchunguzi wa kina kuusiana na tukio hilo.

“Tunaomba matukio haya yakomee hapo na yasiendelee kama kuna waganga wanaendelea kufanya matukio kama haya chama cha waganga UWAWATA tutaendelea kufatilia ili atakayebainika achukuliwe hatua lakini kama kuna watu wengine wanafanya hivi ili tuonekane waganga sisi ni wabaya basi serikali ifatilie na kuwakamata ili wachukuliwe hatua” Bujukano Mahungu, Mwenyekiti UWAWATA

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP Safia Jongo alimesema tukio hilo linaonekana ni la kupangwa na jeshi la polisi litawachukulia hatua wote wanaotoa taarifa za upotoshaji juu ya tukio hilo.

“Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua wote wanaopotosha kwa kuchukua taarifa na kuzitengeneza kwa maslahi yao binafsi na kupelekea kuzua taaruki kwenye jamii, niwatoe hofu wenye ulemavu wa ngozi wako salama na mimi kama Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Geita nawahakikishia kwamba wote waliohusika katika tukio hili watakamatwa na kuchukuliwa hatua" alisema SACP Safia Jongo 

"Niwambie wenye ulemavu wa ngozi hamko hatarini mpo salama ni watu tu wanazua taaruki ili msiendelee na shughuli zenu Geita ipo salama na walemavu wa ngozi wapo salama endeleeni na shughuli zenu kama kawaida” amesesitiza SACP Safia Jongo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Geita.