Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wahusika wote wa uchaguzi ikiwemo jeshi la polisi na idara ya uhamiaji kuhakikisha wanatembelea kwenye vituo vya kujiandikisha kupiga kura ili kuwatambua wale wote ambao hawana vigezo vya kupiga kura hasa wale ambao sio raia wa Tanzania
Waziri mkuu ameyasema alipozindua uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, katika uwanja wa Kawawa, mkoani Kigoma ambapo amesema uchaguzi ujao tofauti na miaka mingine wafungwa na mahabusu kwa mara ya kwanza watashiriki uchaguzi kwa kupiga kura
Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya watu na Makazi ya Mwaka 2022 jumla ya wapiga kura wapya 5,586,433 wataandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuongeza kuwa wapiga kura hao ni ambao watakuwa wametimiza umri wa miaka 18 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020 baada ya uchaguzi mkuu uliopita na ambao watatimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, inakadiriwa kuwa wapiga kura 4,369,531 wataboresha taarifa zao.
“Idadi hii si ndogo kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura hivyo nitoe rai kwa kila mpiga kura aliyeandikishwa na mwenye uhitaji wa kuboresha taarifa asisite katika vituo vya kujiandikisha tume imejipanga kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa popote walipo mpaka vitongojini”
“Nitoe rai kwa kila mpiga kura aliyeandikishwa mwenye uhitaji wa kuboresha taarifa iwe kwa kurekebisha taarifa au kuhama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda lingine asisite kufika katika kituo cha kuandikisha kwani Tume imeshajipanga ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa” Kassim Mjaliwa - Waziri mkuu wa Tanzania