Jumatatu , 15th Feb , 2016

Wafanyakazi 13 wa kampuni ya Kyaka Ranching mkoani Kagera wamenusika kifo baada ya kukatwa katwa mapanga na kundi la wafugaji waliovamia kambi ya kampuni hiyo

Sehemu ya uharibifu inayodaiwa kufanywa na wafugaji hao

Wafanyakazi 13 wa kampuni ya Kyaka Ranching mkoani Kagera wamenusika kifo baada ya kukatwa katwa mapanga na kundi la wafugaji waliovamia kambi ya kampuni hiyo baada ya walinzi wa kampuni hiyo kuwazuia kuingiza mifugo yao kwa nguvu kwenye kitalu kinachomilikiwa na kampuni hiyo.

Wafugaji hao wanadaiwa kuvamia kambi hiyo usiku wa kuamkia jana wakiwa na silaha mbalimbali ambazo ni pamoja na mapanga, visu, marungu na mishale na kumnyanganya mlinzi wa kampuni hiyo bunduki aina ya Shortgun na kuondoka nayo.

Wafugaji hao pia wanadaiwa kufanya uharibifu wa mali ikiwa ni pamoja na gari moja na pikipiki tatu na kuondoka na ng’ombe 48.

Mmoja wa wafanyakazi waliojeruhiwa ambaye amelazwa katika hospitali ya nyakahanga ameeleza alivyojiokoa huku Patrick Ishengoma mkurugenzi wa kampuni hiyo, inayomiliki kitalu namba 16 kilichovamiwa akisema kuwa hujuma zinazofanywa na wafugaji wanaoingiza ng’ombe wao kwa nguvu kwenye vitalu wanavyovimiliki zinawakatisha tamaa wawekezaji waliomilikishwa vitalu kwa ajili ya ufugaji wa kisasa hasa wanaotumia mitaji mikubwa katika kuendeleza vitalu hiyo, na kuiomba serikali kutafuta namna ya kutatua tatizo kati yao na wanaovamia vitalu vyao.

Naye, kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Augustine Ollomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo amesema kwa sasa jeshi la polisi linawashikilia watu watatu kwa kuhusika na tukio hilo akiwemo mlinzi wa kampuni hiyo aliyenyanganywa bunduki na linaendelea kuwasaka watu wengine waliokimbia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Augustine Ollomi