Wakiongea katika machinjio ya Rwamishenye mjini Bukoba wafanyabiashara hao wamesema wamegoma kuchinja mifugo hiyo na kutofungua mabucha kabisa kutokana na barua waliyopewa kutoka kwa mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Bukoba, ya kuwataka kupunguza bei ya nyama hali ambayo imepelekea wafanyabiashara kususia barua hiyo na kugoma kuchinja mifugoa yao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa wafanyabiashara hao Haji Yatubu Musa amesema wao hawawezi kuchinja mifugo hiyo kutokana na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika kununua mifugo hiyo na kuisafirisha ambapo amezitaka mamlaka husika kuangalia upya suala hilo na kulitafutia ufumbuzi.
EATV imemtafuta mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya manispaa ya Bukoba Chibunu Lukiku ambapo amedai kwamba leo siyo siku ya kazi na kuwa yeye siyo mchinjaji wa mifugo hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu mkuu wa wilaya ya Bukoba Sporah Pangani amesema ni kweli wafanyabiashara hao walipelekewa barua ya kupunguza bei ya nyama kwa kuwa walipandisha bei kiholela bila kibali kutoka kwenye mamlaka husika hali ambayo imepelekea usumbufu kwa wananchi wa mkoa huo.