Alhamisi , 3rd Dec , 2015

Wafanyabiashara katika soko kuu la majengo lililopo katika manispaa ya Dodoma wametishia kufanya mgomo usiokuwa na kikomo kama Manispaa hiyo itavunja vibanda vya wafanyabiashara walioko pembezoni mwa mto unaopita katikati ya soko hilo.

Hizi ni baadhi ya sehemu za wafanyabiashara wa soko la majengo mkoani dodoma

Mto huo una jumla ya vibanda 100 ambavyo vimejengwa pembezoni na ambavyo vinatakiwa kuondolewa ili gari la kusafisha mto huo uliojaa uchafu (skaveta) liweze kuusafisha.

Agizo la kubomolewa vibanda hivyo limetolewa na kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Dodoma Clemensi Mkusa siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa Jumanne Sagini alipofanya ziara ya kushtukiza ndani ya manispaa na kumtaka mkurugenzi huyo kubomoa vibanda hivyo.

Mkusa amesema kuwa manispaa hiyo imeamua kubomoa vibanda hivyo ili kuiwezesha manispaa hiyo kufanya usafi sokoni hapo na kuweka mazingira ya soko hilo katika hali ya usafi.

Hata hivyo mwenyekiti wa wafanyabiashara sokoni hapo Godson Rwegazama, amepinga hatua ya Manispaa hivyo kubomoa vibanda hivyo kwa kisingizio cha kufanya usafi na kusema kuwa vibanda hivyo viko kihalali kwani manispaa ya Dodoma imekuwa ikikusanya ushuru kila siku kutoka kwenye vibanda hivyo.