Jumapili , 10th Aug , 2014

Baada ya kupinga hatua ya serikali kuwakataza kuingia maeneo ya katikati ya jiji la Dar es Salaam, waendesha piki piki za matairi mawili maarufu kama boda boda pamoja na waendesha bajaji wameibua tuhuma mpya za kutakiwa kutoa rushwa.

Rushwa hiyo kwa mujibu wa waendesha boda boda hao yanatolewa na wasimamizi wa amri hiyo ambapo wamesema mara wanapokamatwa hutakiwa kulipa kiasi kikubwa cha pesa wanazodai kuwa ni sehemu ya rushwa.

Wakizungumza na East Africa Radio, waendesha pikipiki hao kutoka kituo cha mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam, wamesema hali kwa sasa ni mbaya na kwamba hawaelewi sababu ya uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam kuweka amri hiyo waliyodai kuwa imelenga kuwanufaisha watu wachache.

Mmoja wa wendesha pikipiki hao Bw. Denis Pascal amesema kuna nyakati hutakiwa kulipa hadi shilingi laki Nne punde anapoingia na pikipiki yake katikati ya jiji ambapo amehoji uhalali wa fedha wanazotozwa na mantiki ya mtu kutumia pikipiki yake kwa safari na matumizi yasiyo ya kibiashara.

Aidha, Juma moja baada ya EATV kuripoti maji machafu kutiririka katika mitaa ya eneo la Nzasa Mwenge jijini Dar es Salaam, mamlaka katika eneo hilo zimeanza kuchukua hatua kwa kuzibua mitaro iliyoziba na mazingira kuanza kurejea katika hali yake ya kawaida.

Hata hivyo, tatizo sugu limebaki kwa barabara na mitaa jirani na mamlaka ya mapato Mwenge, ambapo KURASA imeshuhudia maji ya chooni yakitiririka kwa wingi barabarani hali inayotishia afya ya wakazi wa eneo hilo kama anavyoeleza mkazi wa Mwenge Nzasa Bw. Ramadhani Duma.