Jumamosi , 6th Feb , 2016

Fursa ya biashara ya zao la mhogo imezidi kukua kwa wawekezaji kutoka nchini china kuonesha nia ya kununua tani milioni mbili za muhogo mkavu kila mwaka

Fursa ya biashara ya zao la mhogo imezidi kukua kwa wawekezaji kutoka nchini china kuonesha nia ya kununua tani milioni mbili za muhogo mkavu kila mwaka na kuahidi kuongeza nusu zaidi ya kiasi hicho kila mwaka iwapo wataridhishwa na upatikanaji wa uhakika wa mhogo ulio bora.

Wachina hao, wamefika nchini kujiridhisha kuhusu upatikanaji wa muhogo bora na wa uhakika, ili wapate muhogo mkavu watakaousafirisha kwenda nchini mwao kwa matumizi mengine.

Mratibu wa zao la mhogo kitaifa, Dk Geofrey Mkamilo, amesema ni fursa kwa wakulima kuhakikisha wanalima mbegu bora zilizofanyiwa utafiti, ambazo zina uwezo wa kuzaa kati ya tani 20 hadi 30 za muhogo mbichi kwa hekta ikilinganishwa na mbegu za kienyeji. Ambazo uwezo wake ni mdogo, na zimekuwa hazihimili magonjwa sugu ikiwemo michirizi ya kahawia na bato bato kali.

Amesema kwamba uwezo wa sasa wa uzalishaji muhogo nchini bado uko chini kufikia matarajio ya wawekezaji hao sambamba na wengine wakiwemo wa nchini ufaransa wanaotaka kuanzisha kiwanda cha kutengeneza wanga mkoani Lindi.

Katika wilaya ya Newala, mkoani Mtwara, katika kituo kidogo cha utafiti wa majaribio cha Mtopwa, baadhi ya wananchi wanaolima mihogo, wameeleza matumaini yao katika kilimo cha muhogo, baada ya kubaini uzaaji bora na wenye tija wa mbegu zilizofanyiwa utafiti, ukilinganisha na zile za asili ambazo wamekuwa wakizitumia