
Wakulima wakiwa katika uuzaji wa mavuno yao
Akiongea na EATV katika mahojiano maalum hii leo jijini Dar es Salaam kuhusiana na hatua ambazo Wizara hiyo inazichukuwa katika kuimarisha na kuboresha vyama vya ushirika nchini na kuondoa ubadhirifu Mrajisi Mkuu wa serikali Dkt. Audax Peter Rutabanzibwa amesema kumekuwa na viongozi wanaotumia nafasi zao vibaya na kuwalagai wakulima kuachana na mfumo wa stakabadhi galani.
“Stakabadhi ghalani inalenga kumnufaisha mkulima asilimia 100 sasa hawa viongozi wanaokataa stakabadhi ghalani wana ajenda gani? Kwanini wanataka kuirudisha nyuma serikali katika juhudi za kuwanufaisha wakulima ili apate pesa kulingana na stahiki yake” amesema
Dkt. Audax amesema katika kuhakikisha mfumo wa stakabadhi ghalani unatumika kikamilifu na kulingana na sheria iliyotungwa na Bunge kuhusiana na mfumo huo tutawachukulia hatua za kisheria viongozi ambao wanakataa mfumo huo maana lengo lao ni kuwafilisi wakulima.
“Kuna watu wanaitwa KANGOMBA hawa wanawarubuni wakulima na kuwauzia mazao kwa bei ya hasara, tutawadhibiti hasa ukizingatia mikakati mipya ya Serikali tunayoifanya ni lazima tuwabane wasiwaibie wakulima wetu ili wanufaike na jasho lao” amesema
Aidha Dkt. Audax amesema kuwa wanabadili mfumo wa vyama vya ushirika na kwa kukusanya mazao na kuyaongezea thamani mazao kabla ya kuingia sokoni ili kuendana na dhana ya viwanda kwa mazao ya biashara na aina nyingine ili kuwanufaisha wakulima
Mfumo wa stakabadhi ghalani umeonesha mafanikio makubwa kwa sekta ya kilimo nchini Kenya na mataifa mengine yaliyoendelea katika kilimo duniani kwani mfumo huo unawawezesha wakulima kuuza kulingana na bei iliyopo sokoni na siyo kuwafaidisha wanunuzi wa kati hivyo serikali itazingatia hilo ili kupiga hatua kimataifa.