Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) , Dkt. Fatma Mrisho
Wakizungumza na kituo hiki katika mtaa wa Hagafilo mjini Njombe baadhi ya waathirika hao wamesema kuwa wamekuwa wakinyanyaswa kwa kutukanwa pindi wanapoenda kuchukua dawa kwenye vituo vya kutolea huduma hiyo jambo ambalo limekuwa likisababisha watu wengi kukata tamaa ya kuendelea kutumia dawa.
Wamesema kwenye baadhi ya vituo vya kutolea huduma hiyo kumekuwepo na wahudumu ambao hawana nidhamu nzuri kwa mgonjwa ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa baadhi yao ambapo wamekuwa hawana uzoefu katika kuwahudumia wagonjwa hao.
Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na utoaji huduma kwa wagonjwa wa VVU majumbani la SHISO katika halmashauri ya mji wa Njombe Isaya Madembwe amepongeza hatua ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kubadili matumizi ya fedha zilizopangwa kutumika katika maadhimisho ya UKIMWI na kutaka kununulia dawa.
Kwa upande wake mhudumu wa wagonjwa wa virusi vya UKIMWI majumbani katika kata ya Mjimwema Steven Mturo ametumia fursa hiyo kuwataka watumishi wenye tabia ya kuwadharau wagonjwa kuachana nayo kwani imekuwa kazi ngumu kuwarejesha pindi wanaposusa kuendelea kutumia dawa za VVU.
Desemba mosi ya kila mwaka ni siku ya maadhimisho yaUKIMWI duniani ambapo kwa mwaka jana maadhimisho hayo kitaifa yalifanyika mkoani njombe huku kwa mwaka huu kabla hayajaahirishwa yalipangwa kufanyika mkoani Singida.