Jumamosi , 10th Jan , 2015

Kaya 105 za Waathirika wa mafuriko katika maeneo ya Magole na Mateteni wilayani Kilosa zimepatiwa msaada wa bati 1,155 kutoka shirika la kimataifa la SAVE THE CHILDREN yenye thamani ya shilingi milioni 16.5 ambapo kila kaya imeweza kupata bati 14.

Akizungumza wakati wa kukabidhi bati hizo afisa kutoka shirika la SAVE THE CHILDREN nchini Peter Nyaluke amesema msaada huo utatolewa kwa waathirika wa kaya 35 kambi ya Magole na kaya 70 kambi ya Mateteni.

Amesema awali walitoa msaada wa Mablanketi, sabuni, Godoro, Sola, na Mikeka na baadaye Seti za vyombo vya ndani, Mbolea, Majembe na Mashoka kabla ya sasa kuamua kutoa bati.

Akipokea msaada huo,Mkuu wa wilaya ya Kilosa Elias Tarimo amesema bati hizo zitawalenga waathirika ambao hawajapata kabisa bati, kwani kuna baadhi yao walishapatiwa bati kutoka serikalini kupitia ofisi ya waziri mkuu tawala za mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT.

Tarimo amesema bati hizo zitasaidia waathirika hao kujenga nyumba za kudumu na kwamba mpaka sasa wilaya hiyo imeanza zoezi la upimaji viwanja kwa ajili ya kuwagawia waathirika walio kwenye kaya 520 waliokumbwa na mafuriko hayo.