Zaidi ya familia 665 za waathirika wa mafuriko ya Magole wilayani Kilosa mkoani Morogoro wamelalamikia kuishi katika mazingira magumu baada ya mahema wanayoishi kutoboka na kunyeshewa na mvua na kushindwa kulala usiku kutokana na maji kujaa na kutupia lawama serikali kuchelewa kutimiza ahadi ya kuwapatia mabati baada ya nyumba zao kubomoka na kusombwa na mafuriko.
Wakizungumza kwa masikitiko wananchi hao wakiwemo wanawake na watoto pamoja na wazee huku wakionesha mahema yalivyochakaa na kutaabika na mvua na jua kali wananchi hao wamenyooshea vidole baadhi ya viongozi wa serikali ya wilaya kuwabagua na kugawa mabati yaliotolewa na serikali kwa baadhi ya yao na wengine kuachwa huku baadhi ya wazee wakilia hawajua nini hatma ya maisha yao.
Akizungumza na wananchi hao baadhi ya wasamaria wema waliowatembelea waathirika hao Alhaj Mubarak Bawazir ameahidi kutoa msaada wa mabati kuwezesha wananchi hao kurudi katika makazi yao ya kawaida huku baadhi ya watendaji wa chama cha mapinduzi kata ya magole wakikiri kuwa wananchi hao wanateseka kwa kukosa huduma mbalimbali zikiwemo za afya na kwa zaidi ya miezi Sita hawana huduma ya maji katika kambi hizo.