Waandishi wa habari wakitekeleza majukumu yao katika moja ya mikutano.
Wito huo umetolewa leo Jijini Arusha na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Husna Mwilima kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Arusha, Daudi Ntibenda, wakati alipokuwa akifungua mkutano wa siku mbili wa kujadili masuala ya ulinzi na usalama kuelekea uchaguzi mkuu, ulioandaliwa na mtandao wa utetezi wa haki za binadamu.
Amesema waandishi wana nafasi kubwa ya kuelemisha umma madhara ya vita hasa wakati huu, kabla ya uchaguzi mkuu, ili wananchi waepukane na masuala ya vurugu wakati wa uchaguzi.
Pia amesema ni vema kila mwandishi wa habari akaepukana na masuala ya kushabikia vyama vya siasa anavyopenda ili kuhakikisha Tanzania inabaki kisiwa cha amani.
Mwilima amesema kwa sasa kuna kila dalili za viasharia vya kutoweka kwa amani, maana kumezuka malumbano kwa baadhi ya watu kulumbana, hali ambayo siyo nzuri.
Aidha amewaomba viongozi wa vyama vya siasa, dini na taasisi zisizo za kiserikali kushirikiana kueleza wafuasi wao juu ya umuhimu wa kutunza amani wakati wa uchaguzi mkuu.
Naye mwakilishi kutoka taasisi ya kuhamasisha masuala ya amani nchini Marekani, Steve Hege amesema wao wanafadhili nchi 12 za bara la Afrika zenye machafuko, ila kwa Tanzania wameamua kufadhili mtandao huo ili uanze kutoa elimu juu ya umuhimu wakutunza amani, ili sifa iliyopo ya kisiwa cha amani isitoweke.
Amesema amani nyingi katika nchi mbalimbali na hasa Afrika zinatoweka mara baada ya uchaguzi mkuu, hivyo vema kila mwananchi akalinda amani na usalama wa kila mtu.