Jumatano , 23rd Nov , 2016

Vyuo vya Elimu ya Juu vya Afrika Mashariki na Kati vimekutana kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam, kutathmini namna ambavyo vinachangia maendeleo ya nchi zao sambamba na kuondoa idadi kubwa ya wahitimu wasiokidhi mahitaji ya soko la ajira .

Wahitimu

Lengo la mkutano huo, ni kujadili mbinu ambazo zitawezesha vyuo vikuu kuondokana na uwezo mdogo wa wanafunzi wanaohitimu kushindwa kubuni mbinu za kutatua changamoto za kimaendeleo na kuongeza ari ya ubunifu miongoni mwao kwani tatizo la wahitimu kutoajiriwa linaathari hasa katika maendeleo ya viwanda na kuzalishaji.

Balozi Ramadhani Mwinyi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema licha ya kuwepo kwa tatizo hilo ni vyema vyuo vikuu vitajikita katika kuwaelimisha wahitimu kutumia fursa za kiraslimali zinazowazunguka.

Mkurugenzi wa Baraza la Biashara Afrika Mashariki Bi. Lilian Awinja amesema, viwanda vingi vinaajiri wahitimu wasioweza kuendesha mitambo ya uzalishaji hivyo ni vyema vyuo vikajadili namna ambavyo elimu wanayotoa itaendana na mahitaji ya sasa ya kiuchumi kuliko kung'ang'ania mifumo isiyo na tija katika uchumi.