Jumanne , 29th Sep , 2015

Vyuo vikuu 16 vya nchi za Afrika, vimekutana jana Jijini Arusha, kupanga mikakati jinsi ya kuwasaidia vijana wanaohitimu katika vyuo hivyo, waweze kujiajiri katika ujasiliamali, badala ya kusubiri ajira.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa kwanza wa Umoja wa wa vyuo vikuu vya Afrika.

Akizungumza leo Jijini hapa, katika warsha ya siku tatu, iliyoandaliwa na Umoja wa Vyuo Vikuu vya Afrika (AAU), Chuo cha Mzumbe na Afrika Kusini, kwa niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo, Dk. Shukuru Kawambwa, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya juu Tanzania, Chacha Musabi, amesema warsha hiyo imekuja wakati muafaka, kwani vijana wengi wakihitimu wanashindwa kujiajiri wenyewe kwa sabu vyuo haviwaandai kwa ujasiliamali.

Amesema kila chuo ipo haja kutilia mkazo katika elimu ya ujasiliamali na kuwafundisha kwa vitendo, ili waweze kujiajiri wenyewe, mara baada ya kuhitimu elimu vya vyuo vikuu.

Dk. Kawambwa amesema ipo haja vyuo hivyo, vikabadilika kwa haraka kwa kubuni njia za kuwasaidia vijana hao, ili waweze kujipatia kipato nje ya ajira.

Naye Kaimu Makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha Mzumbe, Prof. Itika Josephat, amesema warsha hiyo imealika watendaji wa kati wa vyuo vikuu vya Afrika, ili wazungumzie na kubadilishana uzoefu juu ya kufundisha vijana wa vyuo hivyo elimu ya ujasiliamali kwa ajili ya kuwaondoa katika utegemezi wa ajira pekee.