Akizungumza na wajasiriamali mkoani Lindi Makamu wa Rais amesema kuna madawati mengine yanapopelekwa mashuleni hayadumu kutokana na utengenezaji wake kuwa wa hali ya chini jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada za serikali katika kumaliza changamoto ya madawati mashuleni.
''Ninawapongeza Mkoa wa Lindi kwa jitihada ambazo mmechukua kukabiliana na tatizo la madawati ambapo sasa mmebakiza asilimia moja, jambo la msingi ambalo nawaagiza viongozi na watendaji husika ni kuhakikisha wanasimamia vyema utengenezaji wa madawati hayo'' Amesema Makamu wa Rais.
Aidha katika kusisitiza hilo Makamu wa Rais amesema suala la madawati linatakiwa kumalizika ili serikali ianze kujikita katika masuala mengine muhimu ya sekta ya elimu ikiwemo mishahara ya walimu, madarasa, maabara na mambo mengine, ili hadi mwaka 2020 sekta ya elimu iwe imepiga hatua.
Kuhusu kero ya riba katika taasisi za fedha ambazo zinawakabili wajasiriamali Makamu wa Rais amesema jambo hilo serikali inalifahamu na inalifanyia kazi kwa kuwa siyo jambo la kuamka na kupunguza riba kwa siku moja bila wadau hasa Benki Kuu kutazama suala hilo na namna linavyoweza kusaidia au kuathiri mfumo wa fedha nchini.





